Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango ameiomba Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA), kusaidia upatikanaji wa fedha kwa njia ya mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ikiwemo Reli ya kisasa, Nishati na Kilimo.
Dkt Mpango ametoa ombi hilo jijini Dodoma, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa JICA Dkt Nobuko Kayashima, ambapo Viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa miradi inayokusudiwa kufadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika hilo.
Amesema kuwa hivi sasa Serikali imeelekeza nguvu na fedha zake za ndani kujenga Reli kwa kiwango cha kisasa (SGR), ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme kwa njia ya maporomoko ya maji ya Mto Rufiji mkoani Pwani, na kwamba miradi hiyo inahitaji fedha nyingi ambazo anaamini Japan inaweza kusaidia upatikanaji wake.
“Tumeanza kutekeleza miradi hii kwa kutumia fedha zetu za ndani na tunaiomba Serikali ya Japan kuzishawishi taasisi zake za fedha kwa kushirikiana na Taasisi nyingine kutupatia mikopo yenye masharti nafuu ili tuweze kukamilisha miradi hiyo muhimu kwa Taifa” amesema Dkt Mpango.
Amefafanua kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza shughuli za kiuchumi na kibiashara hapa nchini pamoja na nchi jirani ambazo hazijapakana na bahari, huku nishati ya umeme ikitarajiwa kuboresha upatikanaji wa umeme kwa ajili ya kuendesha Reli hiyo pamoja Viwanda.
Aidha Dkt Mpango amemuomba Kiongozi huyo wa JICA kuisaidia Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Serikali kuendeleza rasilimali watu ama nguvu kazi kwa kuwapatia fursa ya masomo nchini Japan wataalam kutoka Wizara yake na maeneo mengine Serikalini, ili kuongeza ubobezi wa wataalam hao katika sekta ya Uchumi, Fedha, pamoja na Tiba hasa matibabu ya moyo na figo.
Akijibu maombi ya Waziri Mpango, Makamu huyo wa Rais wa JICA Dkt Nobuko Kayashima amekubali kusaidia kuendeleza rasilimali watu, ambapo kwa kuanzia Shirika hilo limeahidi kutoa nafasi ya Watumishi 15 kutoka Wizara ya Fedha na Mipango na Sekta nyingine kupata ufadhili wa masomo nchini Japan.
Amesema kuwa, Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa litaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya Wananchi, ambapo miradi mipya inayokusudiwa kufadhiliwa na Shirika hilo ni ule wa upanuzi wa Bandari ya Kigoma, Ujenzi wa Barabara ya Arusha – Holili na mradi wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Zanzibar.