Jaji Mkuu : Tujadili hatma ya ajira

0
107

Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma amesema kuna umuhimu wa kujadili hatma ya ajira ya tasnia ya sheria katika karne ya 21, kutokana na kuwepo kwa changamoto za ajira kwa mawakili.

Jaji Mkuu ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika sherehe ya 67 ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya 358 iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee mkoani Dar es Salaam.

Amesema katika mazungumzo yake aliyoyafanya na mawakili hao wapya amegundua wengi wao hawajui watapata wapi ajira, hivyo changamoto hiyo inahitaji majadiliano ya kina baina ya mhimili wa mahakama na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) pamoja na mamlaka nyingine.

Ameongeza kuwa anaamini serikali itaendelea kuwekeza katika miradi itakayoibua fursa za ajira kwa Mawakili huku akitoa wito kwa mawakili hao wapya kujitathmini ni kwa namna gani watanufaika kiajira na fursa zilizopo ikiwemo ile ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.

Jaji Mkuu amesema kupitia maboresho ya kiteknolojia yaliyofanyika katika mahakama za wilaya nchini, mawakili wapya hawana budi kuchangamkia fursa hiyo kwa kufungua ofisi za Mawakili katika wilaya hizo.

Aidha, amewakumbusha Mawakili nchini kuwa uwakili ni uadilifu, uaminifu, uwezo, umahiri, unyoofu na huduma bora ili kutunza sifa ya tasnia ya sheria na mahakama kwa ujumla.