Serikali imewataka wananchi kuepuka kuingiza nchini na kutumia majokofu au viyoyozi vilivyokwishatumika (mtumba) ambavyo vinatumia gesi haribifu kwa tabaka la ozoni na badala yake watumie bidhaa zenye uwezo mdogo wa kuchangia ongezeko la joto duniani.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi Ya Makamu Wa Rais (Muungano Na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo, wakati akitoa Tamko kuhusu Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni jijini Dodoma.
Amesema hayo wakati Tanzania ikitarajia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni, Septemba 16, 2023, kama kumbukumbu ya tarehe ya kutiwa saini Itifaki ya Montreal ya mwaka 1987 kuhusu kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni, ambalo kazi yake ni kuchuja sehemu kubwa ya mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia.
Dkt. Jafo amesema tabaka la ozoni linapoharibiwa husababisha saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi, kujikunja kwa ngozi, kuathirika kwa ukuaji wa mimea pamoja na kuongezeka kwa joto duniani na hivyo kuchangia katika mabadiliko ya tabianchi.
Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka huu ni “Hifadhi ya tabaka la ozoni na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi,” ambayo imechaguliwa kutokana na mafanikio ya kimataifa kupitia utekelezaji wa Itifaki ya Montreal katika kuchangia jitihada za kuhifadhi tabaka la ozoni na kupunguza athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.