ILE MIKOPO YA HALMASHAURI IKAWASAIDIE HAWA

0
181

Rais Samia Suluhu Hassan ameilekeza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na mamlaka nyingine kuandaa mpango utakaowawezesha waraibu wa dawa za kulevya kupata mitaji ili wasikose kazi za kufanya pale wanaporejea katika familia zao baada ya kupona.

Rais Samia ameyasema hayo alipokuwa akihutubia katika maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani yaliyofanyika mkoani Arusha.

Rais Samia ametoa maelekezo hayo baada ya mtu mmoja aliyepona uraibu wa dawa za kulevya kuiomba Serikali iwakumbuke kwani wanapopona na kurejea kwenye familia zao hukosa shughuli za kufanya na hivyo kurudia hali za awali au kujihusisha na vitendo viovu ili kujikimu kimaisha.

“Nilikuwa nanong’ona na Waziri Mkuu, wazo la kwamba zile fedha tulizozisitisha za halmashauri zile asilimia kumi….. Mmewasikia hapa wanalalamika kwamba tukishapoa hatuna cha kufanya……
Sasa ile asilimia kumi Waziri Mkuu atakaa na TAMISEMI na wengine wanaohusika kuzielekeza halmashauri kuja na mpango mzuri kama ni kupitia benki au vyovyote lakini vijana hawa waunganishwe na halmashauri wafikie ile asilimia kumi. Hasa ile asilimia nne ya vijana kama ni Wanaume na kama ni Wanawake asilimia nne ya Wanawake waende wakapate wajue kile wanachokwenda kukifanya ….. “.

“…….na hiyo ni pamoja na jitihada za Serikali za kuwasomesha, ikiwezekana kuwapatia vifaa na kuwapatia mtaji wa kwenda kufanya kazi zao”. Ameelekeza Rais Samia