Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro amewaongoza Makamishna na Maofisa Wakuu Waandamiazi wa Jeshi hilo katika zoezi la usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole, linaloendeshwa kupitia kampuni mbalimbali za simu za mkononi nchini.
Akizungumza kabla ya kufanyika kwa zoezi hilo, IGP Sirro amesema kuwa, usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole utasaidia katika kubaini uhalifu na wahalifu, na kwamba hakuna mtu atakayeweza kujificha pale atakapojihusisha na uhalifu ukiwemo ule wa kimtandao.
IGP Sirro ametumia usajili huo wa laini za simu, kuwataka wafanyakazi wa kampuni za simu nchini kuwa waaminifu wakati wanapotekeleza majukumu yao, na kujiepusha kujiingiza kwenye matukio ya uhalifu.