IGP Sirro atoa kauli kupatikana kwa MO

0
2257

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro amewaomba Watanzania wote kuwa watulivu wakati vyombo vya ulinzi vikiendelea na uchunguzi wake kuhusiana na tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji maarufu kama MO.

IGP Sirro ametoa ombi hilo jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari, saa kadhaa baada ya mfanyabiashara huyo kupatika katika eneo la viwanja vya Gymkana jijini Dar es salaam saa nane usiku wa kuamkia hii leo.

Ameongeza kuwa vyombo vya ulinzi linaendelea kuifanya kazi hiyo kwa umakini mkubwa na kwamba wamekwishawabaini watuhumiwa ikiwa ni pamoja na dereva wa gari iliyotumika ambayo nayo ilitelekezwa katika eneo hilo la Gymkana.

Ametoa wito kwa Watanzania kupuuza maneno ya baadhi ya watu kuwa vyombo vya ulinzi na usalama havijafanya jitihada za kutosha za kufanikisha kupatikana kwa MO.

Mkuu huyo wa Jeshi la Polisi nchini amesisitiza kuwa wote waliohusika katika tukio hilo hilo lazima watakamatwa hata kama wapo nje ya nchi, kwa kuwa jeshi hilo lina mawasiliano na mamlaka mbalimbali ambazo zinaweza kufanikisha jambo hilo.

MO alitekwa Oktoba 11 mwaka huu na watu wasiofahamika katika hoteli ya Collessium iliyopo jijini Dar es salaam alikokwenda kufanya mazoezi.