IGP : Shule za udereva zikaguliwe

0
103

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura ameagiza kufanyika kwa ukaguzi kwenye vyuo vinavyotoa mafunzo ya udereva hapa nchini, ili kujiridhisha kama bado vina uwezo wa kutoa elimu hiyo.

Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani inayofanyika Kitaifa mkoani Mwanza, IGP Wambura amesema, ukaguzi huo uzingatie elimu inayotolewa na vyuo hivyo, viwango vya walimu wanaotoa elimu na mitaala ya udereva.

IGP Wambura amesema, ubora wa madereva utasaidia kupunguza ajali za barabarani kwa kiwango kikubwa, hivyo pamoja na ukaguzi wa vyombo vya moto lakini pia kufanyike ukaguzi kwenye vyuo vya udereva.

Ameongeza kuwa lengo la Jeshi la Polisi nchini ni kudhibiti ajali za barabarani kwa kuweka usimamizi kwenye kila eneo linalotumia barabara na usimamizi wa sheria kwa ujumla.

Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani yanafanyika mkoani Mwanza kuanzia lleo Machi 14 , 2023 hadi Machi 18, 2023 yakiwa na kauli mbiu inayosema kuwa “Tanzania bila ajali inawezekana, Timiza Wajibu Wako”.