Serikali ya Finland inatarajia kutoa Euro 9.5 sawa na Shilingi Bilioni 24, kwa ajili ya mradi wa awamu ya Pili wa Panda Miti Kibiashara utakaodumu kwa muda wa miaka minne kwa ajili ya Wakulima wadogo wa miti wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Akizindua awamu ya Pili ya mradi huo huko Mafinga wilayani Mufindi mkoani Iringa, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu ameiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ambayo ndiyo msimamizi Mkuu wa mradi huo kwa niaba ya Wizara, kuusimamia vizuri.
Naibu Waziri Kanyasu amewataka Wataalamu wote watakaokuwa kwenye utekelezaji wa mradi huo wa awamu ya Pili wa Panda Miti Kibiashara, kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotolewa.
Katika awamu ya kwanza ya mradi huo, Finland ilitoa Euro Milioni 19.5 sawa na Shilingi Bilioni 40 kati ya mwaka 2014 na 2018, ambapo kupitia uwezeshaji huo jumla ya hekta Elfu 12 za miti bora zimepandwa na zinamilikiwa na Wananchi zaidi ya Elfu Tisa.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo wa Maliasili na Utalii ameishukuru Serikali ya Finland kwa kufadhili mradi mwingine wa kuongeza mnyororo wa thamani kwa mazao ya misitu uitwao FORVAC, mradi unaotekelezwa na wizara hiyo katika wilaya Kumi za mikoa ya Tanga, Dodoma, Lindi na Ruvuma.
