Hukumu ya viongozi wa CHADEMA inaendelea kusomwa

0
395

Hukumu ya kesi inayowakabili viongozi waandamizi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), pamoja na aliyekua Katibu Mkuu wa Chama hicho Dkt Vicent Mashinji inaendelea kusomwa hivi sasa katika Mahakama ya Halimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es salaam.

Mwandishi wa habari wa TBC aliyepo katika Mahakama hiyo kufuatilia hukumu hiyo amesema kuwa, ulinzi umeimarishwa katika maeneo yote ya Mahakama hiyo.

Viongozi hao wanatuhumiwa kutenda makosa 13 ikiwa ni pamoja na kufanya kusanyiko na maandamano kinyume na sheria na kutoa maneno ya kichochezi katika siku ya kufunga kampeni za uchaguzi wa marudio kwenye jimbo la Kinondoni mkoani Dar es salaam mwaka 2018.

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, Katibu wa CHADEMA Taifa John Mnyika, Mbunge wa jimbo la Kawe Halima Mdee, Mbunge wa Bunda Mjini Ester Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko, Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini John Heche na Mbunge wa jimbo la Iringa Mjini Peter Msigwa.