Hukumu ya kesi ndogo ya kina Mbowe kutolewa leo

0
140

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi iliyopo mkoani Dar es Salaam, leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi namba 16 ya mwaka 2021 inayomkabili Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Hukumu hiyo ni juu ya mapingamizi ya upande wa utetezi unaoongozwa na Peter Kibatala ambao ulipinga maelezo ya mshtakiwa wa tatu Mohamed Ling’wenya pamoja na vielelezo ambavyo ni sare za Jeshi katika kesi hiyo yasipokelewe na mahakama kutokana na kile walichodai kukiukwa kwa taratibu za kisheria katika mwenendo wa kesi.

Miongoni mwa sababu zilizosababisha Mawakili wa utetezi kupinga Mahakama isipokee maelezo na sare za Jeshi zilizokamatwa kwa mshtakiwa Mohamed Ling’wenya ni kwamba Mawakili hao walidai mshtakiwa huyo hakuwahi kupelekwa kituo cha Polisi Central Dar es Salaam kwa ajili ya kuchukuliwa maelezo baada ya kusafirishwa kutoka Moshi mkoani Kilimanjaro.

Pia mawakili hao walidai Mshitakiwa Mohamed Ling’wenya alitishiwa ili aweze kusaini maelezo yake akiwa katika kituo cha Polisi cha Tazara na kwamba baada ya kutolewa kituoni hapo na kupelekwa kituo cha polisi Mbweni aliteswa.

Katika kesi ya Msingi Mbowe na wenzake wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya ugaidi,wanayodaiwa kuyafanya katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Kilimanjaro na Morogoro.