Naibu waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema, matibabu ya ugonjwa wa Fistula kwa sasa yanatolewa katika hospitali zote za kanda na kwamba wagonjwa hawalazimiki kufuata matibabu hayo katika hospitali ya CCBRT mkoani Dar es Salaam.
Dkt. Mollel ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Aleksia Kamguna ambaye alitaka kufahamu mkakati wa serikali katika kuongeza wigo wa upatikanaji wa matibabu ya ugonjwa wa Fistula katika maeneo ya karibu na wananchi.
Akijibu swali hilo Dkt. Mallel amesema, serikali imepeleka wataalamu katika hospitali za kanda ili kutoa matibabu ya ugonjwa huo kwa wananchi, na hivyo kuwawezesha wananchi wenye matatizo ya ugonjwa huo kutibiwa kwa wakati na katika maeneo ya karibu.