Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam na Pwani (DAWASA) imefanikiwa kusambaza maji kwa wakazi wa mikoa hiyo kwa asilimia 92 mpaka sasa.
Akitoa tathmini ya utendaji kazi wa mamlaka hiyo mbele ya Waziri Jumaa Aweso, Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema bado mamlaka hiyo inaendelea kusambaza huduma ya maji kwa maeneo ambayo wanayahudumia ikiwemo kununua mitambo ya kisasa ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi.
Akitoa tathmini yake, Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameipongeza mamlaka hiyo kwa kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa meneo ya Dar es Salaam na Pwani na kuwataka waendelee kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji ili ajenda ya kumtua ndoo mama kichwani ifanikiwe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya DAWASA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Devis Mwamunyange amesema kwa sasa mamlaka hiyo inaendelea na uboreshaji wa huduma, ikiwemo kufungua mikoa mipya ya kutoa huduma.