Hospitali ya PUIH yaanzisha ushirikiano na MOI

0
548

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Ubongo na Mishipa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking (PUIH) iliyopo Beijing nchini China,- Profesa Zhao Yuanil.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Profesa Yuanil aliongozana na timu ya wataalamu wanaoshirikiana na Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI).

Wakati wa mazungumzo hayo, Rais Magufuli ameishukuru PUIH kwa kukubali ombi lake la kuanzisha ushirikiano na MOI na amemhakikishia Profesa Yuanil kuwa serikali ipo tayari kutoa ushirikiano zaidi utakaowezesha MOI kuongeza uwezo wake wa kutoa huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania ambao wamekuwa wakikosa huduma hiyo ama kulazimika kutumia gharama kubwa kwenda nje ya nchi.

Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za kufanyika kwa mafanikio upasuaji wa kwanza uliofanywa na Profesa Yuanil na kwamba anaamini wataalamu zaidi wataendelea kuja nchini kutoka PUIH kwa ajili ya kutoa huduma na kuwafundisha madaktari wa Tanzania na pia Watanzania wengi watakwenda nchini China kujifunza upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.

Kwa upande wake Profesa Yuanil amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuhakikisha MOI inaimarishwa ikiwemo kufanya uwekezaji mkubwa katika miundombinu na amemhakikishia kuwa PUIH itahakikisha makubaliano yaliyotiwa saini mwaka 2018 kati ya hospitali hiyo na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto yanatekelezwa kikamilifu.

“Tanzania kuna watu zaidi ya Milioni 50 na kuna idadi kubwa ya watu wenye magonjwa ya ubongo, wanaopata majeraha kichwani, uvimbe wa ubongo, matatizo ya mishipa ya damu ya ubongo na magonjwa ya uti wa mgongo ambao wanahitaji kupata matibabu mazuri hapahapa, lakini naambiwa kuna wataalamu 10 tu ambao hawatoshelezi mahitaji, ndio maana tupo hapa kuangalia mnafanya nini na tuone namna ya kusaidia kuwaongezea uwezo”, amesema Profesa Yuanil.

Naye Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amemshukuru Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuwatafuta Madaktari Bingwa kutoka PUIH na kutoa maelekezo ya kuanzishwa kwa ushirikiano na MOI, pamoja na kuhakikisha serikali inatoa zaidi ya Shilingi Bilioni 12.5 za kuimarisha miundombinu ya MOI ili itoe matibabu ya kibingwa ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa Watanzania wengi.

“Kwa kweli Watanzania wawe na matumaini makubwa kuwa huduma zile za kibobezi zitapatikana ndani ya nchi na hakuna kwenda nje, mambo yote ndani ya nchi, kwa hiyo tunashukuru sana kwa maono haya ya Rais Magufuli, yeye ndio alipata taarifa kuwa kuna daktari Bingwa huyu wa upasuaji wa ubongo na kisha akatupa maelekezo kuwa daktari huyo ameweza kutoa matibabu kwa wagonjwa walioshindikana katika nchi nyingi, kwa hiyo tukafanya mawasiliano kupitia Ubalozi wetu wa China na baadaye tukasaini mkataba Septemba 2018 nilipokwenda China na sasa tumeanza kutekeleza”, amesema Waziri Ummy Mwalimu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt Respicious Boniface amesema kuwa kupitia ushirikiano huo Tanzania inatarajia kupata wataalamu wengi wa upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu na amebainisha kuwa pamoja na kufanya upasuaji wa mafanikio kwa mgonjwa mmoja, wagonjwa wengine wawili watafanyiwa upasuaji leo na kwamba ushirikiano huu utaiwezesha MOI kuwa kituo bora cha upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu Barani Afrika.