Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imezifungia Hospitali Tatu kutoa huduma ya mionzi (X-Ray).
Sababu za kufungiwa kwa hospitali hizo ni kutokana na kutokidhi matakwa ya sheria namba Saba ya Nguvu za Atomiki ya mwaka 2003 na kwamba vitarejeshewa huduma hiyo mara zitakaporekebisha mapungufu yaliyoonekana.
Hospitali zilizofungiwa kutoa huduma hiyo ya mionzi ni ile ya Sumve, Ngudu na Misungwi, zote ziko mkoani Mwanza.
Hospitali hizo zimefungiwa kufuatia ukaguzi unaoendelea mkoani Mwanza, ukaguzi ambao umekua ukifanyika kila mwaka ili kuhakikisha usalama katika utoaji wa huduma za mionzi unazingatiwa.
Katika hospitali za Sumve na Ngudu imegundulika kuwa Watumishi wake hawana sifa za upigaji wa picha za mionzi huku katika hospitali ya Misungwi imegundulika kuwa vifaa vyao vya mionzi havina ubora unaostahili.
Kufuatia hali hiyo, TAEC inavitaka vituo vyote vinavyotumia mionzi katika utoaji wa huduma mbalimbali, kuhakikisha vinafuata sheria na taratibu za kiusalama kama ilivyoelekezwa katika sheria.