Serikali imeahidi kupeleka vifaa tiba na Wataalamu wa afya kwenye hospitali 67 za wilaya nchini ambazo zinaendelea kujengwa ili kuhakikisha kuwa zinapokamilika zinakuwa na uwezo wa kuwahudumia Wananchi wa wilaya hizo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndungulile ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa Viti maalumu Mariam Kisangi aliyetaka kufahamu namna serikali ilivyojipanga kuhakikisha inazihudumia hospitali hizo pindi zitakapokamilika.
Dkt Ndungulile ameahidi kuwa serikali itahakikisha hospitali hizo zinakuwa na vifaa tiba na Wataalamu wa afya ili lengo la kuzijenga liweze kutimia na kuwahudumia Wananchi.
Amesisitiza kuwa hospitali hizo za wilaya zinazoendelea kujengwa zikikamilika, zitapatiwa vifaa tiba vya kutosha na pia rasilimali watu ili ziweze kuwahudumia Wakazi wa wilaya hizo 67.