HII NI AIBU NA HAIKUBALIKI

0
163

Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni Mwenyeji wa mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) amesema, ni aibu na ni hali isiyokubalika kuelezwa kuwa katika Bara la Afrika wapo watu wanaofariki dunia kwa kukosa chakula.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam katika mkutano wa Mifumo ya Chakula Afrika 2023 (AGRF) unaohudhuriwa na viongozi wakuu wa nchi za Afrika na wadau wa mifumo ya chakula Barani Afrika Rais Samia amesema, inakadiriwa kuwa zaidi ya Waafrika Milioni 283 wanalala na njaa kila siku na wengine wanapata utapiamlo na magonjwa yanayohusiana na lishe huku wengine wakifariki dunia kwa kukosa chakula.

Amesema kutokana na utajiri wa maliasili na fursa zilizopo Barani Afrika, bara hilo lilipaswa kutoa suluhisho kwa changamoto ya mifumo ya chakula duniani kwani Afrika imebarikiwa kwa kuwa na asilimia 65 ya ardhi inayofaa kwa kilimo duniani na watu wake asilimia 60 ni vijana ambao ni nguvu kazi kubwa.

Rais Samia ameongeza kuwa Afrika imebarikiwa kwa kuwa na maji mengi katika mito na maziwa makubwa, pamoja na madini yanayoweza kutoa fedha za kutosha kuwekeza katika sekta ya kilimo.

Amesema licha ya nchi za Afrika kuwa na yote hayo, zimebaki kuwa walalamikaji badala ya kutafuta suluhisho la kuelekea njia ya kuleta Mapinduzi ya uchumi wa kijani.