Heroin yawafikisha kwa Pilato

0
206

Watu wawili wamefikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es salaam  wakikabiliwa na mashtaka mawili, ikiwemo kosa la uhujumu uchumi na kusafirisha dawa za kulevya aina heroin zaidi ya kilo 38.
 
Washtakiwa hao Kenechi Okpala raia wa Nigeria na Aziza Mohammed wamefikishwa na kusomewa hati ya mashtaka katika mahakama hiyo na Wakili wa serikali Kija Luzungana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo Kassian Matembele.
 
Awali kabla ya kusomwa kwa hati ya mashtaka ya kesi namba 97 ya mwaka 2020 inayomkabili Kenechi na mwenzake, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, –  Kassian Matembele alidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi, hivyo washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote mpaka pale Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP)  atakapotoa mamlaka kwa mahakama hiyo kusikiliza shauri hilo.
 
Katika shtaka la kwanza linalomuhusu mshtakiwa namba moja Kenechi Okpala, Wakili wa serikali Kija Luzungana amedai kuwa Novemba 28 mwaka huu alikamatwa maeneo ya Kimara Temboni jijini Dar es salaam akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilo 4.47 kinyume na sheria ya kudhibiti dawa za kulevya.
 
Aidha katika shtaka la pili kwa washtakiwa wote, Wakili wa serikali Luzungana amedai kuwa katika tarehe hiyo hiyo Kenechi na Aziza walikamatwa eneo la Kimara Temboni mtaa wa Upendo wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilo 34.5.
 
Baada ya washtakiwa hao kusomewa mashtaka yao bila kutakiwa kujibu chochote, Wakili Mwandamizi wa serikali Wankyo Simon amedai kuwa  upelelezi wa shauri hilo haujakamilika, hivyo kuomba kupangwa tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
 
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Disemba 23 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote wamerudishwa rumande.