Halmashauri zitoe kipaumbele kuendeleza kilimo

0
128

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe inaweka kipaumbele katika kuwezesha utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs).

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo Machi 2 wakati akizindua mpango wa DADPs katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, jijini Dodoma na kuzitaka taasisi za fedha zijipange kutambua hati miliki za ardhi za wakulima kama dhamana ya kupata mikopo.

Aidha amezielekeza Halmashauri zote nchini kutenga fedha kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kilimo, mifugo na uvuvi ya wilaya.

Ameiagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupitia halmashauri ziendelee kutenga maeneo ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na shughuli nyingine kama vile ufugaji.

“Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Kilimo ziandae na kusimamia utekelezaji wa mkakati madhubuti wa kusimamia utendaji kazi wa maafisa ugani ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo. Maafisa Ugani wasimamiwe kikamilifu ili kuimarisha huduma za ugani kwa wakulima.”