Halmashauri zatakiwa kuongeza kasi katika utoaji hati

0
155

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuanza kujitathmini katika idadi ya hati za ardhi wanazotoa kwa wamiliki wa ardhi kwenye halmashauri zao.

Waziri Lukuvi ameyasema hayo katika mkutano wake wa kusikiliza na kutatua kero za ardhi kwa Wakazi wa mkoa wa Iringa, kupitia programu ya Funguka kwa Waziri.

Ameongeza kuwa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaanza kutangaza wilaya itakayoongoza katika Upangaji, Umilikishaji na Utoaji Hati za ardhi kwa wananchi ili kubaini halmashauri ambazo ziko nyuma katika kutoa hati hizo za ardhi kwa Wananchi.

“Mkurugenzi aone fahari kuwawezesha Wananchi kwa kupima na kuwapatia hati, kama Mkurugenzi huwezi kutoa hati miliki hata Mia Moja basi wewe hufai” amesema Waziri Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, kumilikisha na kumpatia Mwananchi hati ya ardhi ni kumuwezesha kiuchumi kwa kuwa anaweza kuitumia hati kwenye shughuli za kimaendeleo na kusisitiza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanapanga na kuwamilikisha maeneo Wananchi.

Aidha Waziri Lukuvi amesema kuwa kwa sasa wizara yake imejipanga
kuhakikisha inasogeza huduma za ardhi karibu na Wananchi kwa kuanzisha ofisi za mikoa zitakazokuwa na Watendaji wote wa sekta ya ardhi kama vile Wapimaji, Wathamini, Wataalamu wa Mipango Miji pamoja na Wasajili.

“Sasa Wapimaji, Wathamini na Wapangaji watakuja hapa Iringa, muundo unaanza mwezi ujao lengo ni kuwapunguzia usumbufu Wananchi katika kupata huduma za ardhi” amesema Waziri Lukuvi.