Halmashauri zatakiwa kufungua akaunti maalum

0
184

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), – Selemani Jafo ametoa muda kwa mwezi mmoja kwa halmashauri zote nchini, kuhakikisha zinafungua akaunti maalum za Benki kwa ajili ya fedha za maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu.

Waziri Jafo ametoa muda huo wakati akifunga kongamano la Wataalamu wa sekta ya Maendeleo ya Jamii jijini Dodoma na kuwataka kuhakikisha wanasimamia jambo hilo.

“Natoa agizo, ifikapo Novemba 30 mwaka huu kila halmashauri nchini iwe imefungua akaunti maalum ya Benki kwa ajili fedha za Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kwa kuwa fedha zikiendelea kutolewa katika mfumo wa sasa zinakuwa kama zinaelea”, amesisitiza Waziri Jafo.

Ameongeza kuwa fedha hizo zinapotolewa bila ya kuwepo kwa akaunti hiyo maalum, inakuwa vigumu kwa Serikali kuzifanyia tathmini, na hivyo kuwahimiza Wataalamu hao wa sekta ya Maendeleo ya Jamii kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo ili malengo ya kusaidia makundi hayo yaweze kufikiwa.