Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula ameipa mida wa mwezi mmoja halmashauri ya wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, kuhakikisha inatekekeza mradi wa kupima, kupanga na kumilikisha ardhi.
Waziri Mabula ameagiza ifikapo mwisho wa mwezi huu mradi huo uwe umekamilika vinginevyo shilingi milioni 700 kati ya zaidi ya bilioni moja zilozotolewa kwa ajili ya mradi huo zitahamishiwa katika halmashauri nyingine za mkoa huo.
Hatua ya Dkt Mabula inafuatia halmshauri hiyo ya Rombo kushindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, ambapo hadi sasa imefanikiwa kutumia shilingi milioni 60 tu kati ya zaidi ya bilioni moja ilizopewa kwa ajili ya kutekeleza mradi.
Halmashauri ya wilaya ya Rombo iliomba shilingi bilioni 1.060 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika eneo la Holili hasa kitongoji cha Holili shuleni ambapo uchaguzi wa eneo hilo ulizingatia eneo lisilokuwa na maendelezo mengi kuepuka ukuaji holela wa mji.