Halima Mdee: Sisi bado ni CHADEMA

0
501

Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Demokrasia na Mendeleo (CHADEMA), Halima Mdee amesema yeye na wenzake 18 bado ni wanachama wa chama hicho kwani wanakipenda na kukiheshimu.

Mdee akiambatana na wenzake amezungumza hayo mbele ya waandishi wa habari jijini Da es Salaam baada ya kuwepo kwa sintofahamu tangu Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kuwavua uanachama kutokana na madai ya kukiuka taratibu za chama.

“Nimejitokeza hapa kuja kutuliza haya mambo maana yanaonekana ni makubwa ila nimekuja kuyaweka yanavyotakiwa yawe, mimi na wenzangu tumekuja hapa kuzungumza nanyi, na niwaambie sisi ni CHADEMA kindakindaki,” amesema Mdee

Kuhusu tuhuma za kununuliwa, Mdee amesema hajawahi kuwaza kununuliwa na wala hatarajii kwani yeye ni miongoni mwa wabunge waliokuwa wanapinga rushwa ndani ya bunge.

“Kumekuwa na maneno mengi, kuna watu wanasema Halima nimenunuliwa, naomba niseme mimi sijanunuliwa, sinunuliwi na sitarajii kununuliwa.”

Pia amezungumzia madai ya wao kugomea wito wa kamati kuu kama mwenyekiti wa chama hicho alivyosema wakati wa kutoa maamuzi ya kamati hiyo, Mdee amesema waliiandikia barua kuomba wapewe muda ili waweze kwenda wakiwa na majibu ya busara.

“Tuliandika barua wote kuomba muda wa wiki moja ili ituwezeshe kila mmoja wetu tukienda kwenye kikao zile hasira zetu ziwe zimepungua kidogo ili tukifanya maamuzi tusifanye maamuzi yenye hasira kali,” amebainisha mwanasiasa huyo.

Novemba 27 mwaka huu CHADEMA kupitia kwa mwenyekiti wake iliwavua uanachama na nafasi za mbalimbali za uongozi wanachama 19 walioapishwa jijini Dodoma kuwa wabunge wa Viti Maalum kwa madai kuwa walikiuka kanuni na taratibu za chama.