Hali ya upatikanaji wa chakula yaendelea kuimarika : Serikali

0
285

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa, katika kuelekea msimu wa Kilimo wa 2019/2020, hali ya upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuimarika kutokana na uzalishaji mzuri wa mazao ya chakula kwa msimu wa mwaka 2018/2019.

Amesema uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa mwaka 2018/2019 ulifikia Tani Milioni 16.41 ikilinganishwa na mahitaji ya Tani Milioni 13.84 na kuiwezesha nchi kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula kwa asilimia 119. 
 
Akiahirisha mkutano wa 17 wa Bunge jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema kuwa, pamoja na uzalishaji huo mzuri, kumekuwepo na mahitaji makubwa ya nafaka katika baadhi ya maeneo kutokana na hali ya mvua kutokuwa nzuri na kuwepo kwa dalili za kupanda bei za nafaka.

Hata hivyo amesema kuwa, tayari Serikali imetoa maelekezo kwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA), kuhakikisha inasambaza nafaka kwenye maeneo yenye upungufu ili kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei. 
 
“Nitumie fursa hii kuwahimiza Wakulima kutumia vizuri mvua za vuli zinazoendelea kunyesha maeneo mengi ya nchi yetu kwa kupanda mazao yanayostahimili ukame na ekolojia ya maeneo husika, aidha tukumbuke pia kujiwekea akiba ya kutosha ya chakula kwa ajili ya matumizi ya kaya baada ya mavuno badala ya kuuza chakula chote”, amesisiza Waziri Mkuu Majaliwa
 
Kuhusu upatikanaji wa pembejeo, Waziri Mkuu amesema kuwa, katika kuhakikisha Wakulima wanapata mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu, Serikali imetoa bei elekezi kwa mbolea aina ya DAP na UREA ambazo zipo katika mfumo wa ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja.
 
Pia, amezungumzia masoko ya mazao ya Kilimo ambapo amesema licha ya kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini, kumekuwepo na changamoto kadhaa za upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa baadhi ya mazao ikiwa ni pamoja na pamba, korosho na tumbaku.

Bunge limeahirishwa hadi Januari 28 mwaka 2020.