Kwa mwaka wa fedha 2019/20 Halmashauri zilipanga kukusanya shilingi bilioni 765.48 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani na katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 Halmashauri zimekusanya Jumla ya Shilingi bilioni 527.31 ambayo ni asilimia 69 ya makisio ya mwaka.
Uchambuzi wa taarifa za mapato ya ndani ya Halmashauri katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 umeonesha ongezeko la mapato yaliyokusanywa kutoka Shilingi Bilioni 449.82 kwa kipindi cha Julai, 2018 hadi Machi, 2019 na kufikia Shilingi bilioni 527.31 katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 ambalo ni ongezeko la Shilingi bilioni 77 sawa na asilimia 17 .
Vile vile uchambuzi unaonesha kuwa katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 Halmashauri 58 zimekusanya mapato ya ndani kwa asilimia 75 au zaidi kwa kulinganishwa na makisio kwa mwaka wa fedha 2019/20.
Aidha, Halmashauri 96 zimekusanya asilimia 50 au zaidi lakini chini ya asilimia 75 na Halmashauri 31 zimekusanya chini ya asilimia 50 ya makisio ya mwaka.
Halmashauri hukusanya mapato mengi au kidogo kwenye vyanzo tofauti kulingana na hali halisi ya shughuli za kiuchumi za kila Halmashauri ikiwemo mavuno na mauzo ya mazao mbalimbali na katika kipindi hiki ushuru wa Huduma umekusanywa vizuri na umechangia asilimia 26 ya mapato yote katika kipindi cha Julai, 2019 hadi Machi, 2020 na usimamizi wa ukusanyaji wa mapato katika eneo hili unaonekana kuimarika.
Akitoa taarifa ya mapato na matumizi ya Halmashauri Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI Selemani Jafo mapema leo amesema katika kipindi cha miezi tisa (Julai, 2019 – Machi, 2020), Halmashauri ya Mji wa Njombe imevunja rekodi kwa kukusanya mapato kwa asilimia 130 ya makisio ya mwaka 2019/2020 huku Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ikiwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 30 tu ya makisio yake kwa kipindi cha miezi tisa.