Hali ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi yaimarika

0
172

Rais John Magufuli amemjulia hali Askofu Mkuu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi anayepatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Jijini Dar es Salaam.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Magufuli amemkuta Askofu Mkuu Ruwa’ichi akiwa anaendelea vizuri tofauti na hali ilivyokuwa alipomtembelea Septemba 10 mwaka huu, siku aliyofikishwa MOI akitokea hospitali ya KCMC iliyopo mkoani Kilimanjaro alikougua ghafla baada ya kupatwa na ugonjwa wa kiharusi.

Akiwa MOI, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amefanyiwa upasuaji na timu ya Madaktari Bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa mafanikio na sasa anaendelea vizuri.

Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa na kuimarika kwa hali ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi na amewapongeza Madaktari Bingwa wa MOI kwa kumtibu kwa mafanikio makubwa.

Aidha, Rais Magufuli, Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Askofu Mkuu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Padre Alister Makubi wamesali sala ya pamoja ya kumshukuru Mungu kwa uponyaji na kuwaombea wagonjwa wote wapone haraka.

Baada ya kutoka MOI, Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akiwemo Baba Mzazi wa Daktari wa Rais, Mzee Wilson Ngwale.