Graphite kuanza kuchimbwa Ruangwa

0
100

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali ipo katika majadiliano na kampuni ya Uranex kwa ajili ya ujenzi wa mgodi wa madini ya bunyu (graphite) utakaoanza hivi karibuni.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa wananchi wa wilaya ya Ruangwa wajiandae kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi zitokanazo na ujenzi wa mgodi wa graphite.

Ameyasema hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Namikulo, Namkatila na Matambarale katika kata ya Chunyu wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

“Rais Samia Suluhu Hassan amesema kila kwenye rasilimali kabla ya kuanza uwekezaji lazima wahusika wajadiliane na Serikali ili kubaini namna ambavyo itanufaika.” amesema Waziri Mkuu

Waziri Mkuu amesema wakazi wa maeneo hayo watakuwa ndio wanufaika wa kwanza kutokana na shughuli mbalimbali zinakazokuwa zikiendelea kuanzia hatua ya ujenzi hadi uzalishaji.

“Kila shughuli itakayofanyika hapa ni fursa kwetu sisi wana-Namikulo na wana-Ruangwa kiujumla. Tujipange sawa sawa Serikali yenu ipo makini kuhakikisha mnanufaika na mradi huo.” amesisitiza Waziri Mkuu Majaliwa

Kwa upande wake, Meneja wa mradi wa kampuni ya Uranex, Mhandisi Isaac Mamboleo amesema kampuni yao inatarajia kuanza ujenzi wa mgodi huo katika mwaka huu wa fedha.

Amesema mradi huo ambao utahusisha vijiji saba unatarajia kugharimu shilingi bilioni 625 na utazalisha ajira 950 kati yake ajira 600 wakati wa ujenzi na ajira 350 wakati wa uzalishaji.

Mhandisi Mamboleo amesema kwa sasa wanakamilisha ujenzi wa nyumba 59 kwa gharama ya shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kuwafidia baadhi ya wananchi waliopisha ujenzi wa mradi huo.