Ghati ampongeza Rais Samia kwa miradi ya maji

0
156

Mbunge Viti Maalum Mkoa wa Mara (CCM), Ghati Chomete amempongeza Rais wa Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya maji katika mkoa huo.

Ghati ametoa pongezi hizo alipopata fursa ya kuongea na Wananchi katika ziara ya Rais, alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa katika Manispaa ya Musoma.

Amesema awali upatikanaji wa maji ulikuwa ni tatizo katika maeneo mengi mkoani humo, lakini kwa sasa Serikali imeanzisha miradi mingi na mikubwa ya maji ambayo imesaidia kupunguza tatizo hilo.

Ametolea mfano mradi mkubwa wa maji Bukanga ambao tayari unasambaza maji katika mji wa Musoma na baadhi ya maeneo ya pembezoni, mradi wa maji Balima ambao utasambaza maji katika kata za pembezoni mwa Manispaa ya Musoma.

Miradi mingine ni ile ya chujio la maji Serengeti, mradi wa maji Shirati pamoja na ile iliyo chini ya RUWASA katika halmashauri mbalimbali.

Amesema vilio vya akina mama kwasasa vimepungua kwani wengi wamefikiwa na miradi ya maji, hivyo kuiomba serikali kuendelea kusimamia miradi ambayo bado haijakamilika iweze kukamilika haraka.