Gesi asilia kunusuru upungufu wa umeme

0
226

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema linachukua hatua za haraka kwa kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia.
 
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya babari na shirika hilo imeeleza kuwa, hatua hizo zinachukuliwa kutokana na mabadiliko ya hali hewa pamoja na kupungua kwa kiwango cha maji katika mito na mabwawa katika maeneo mbalimbali nchini.
 
TANESCO imetaja hatua hizo za haraka kuwa ni kuongeza uzalishaji kwa kutumia gesi asilia kwa kuharakisha matengenezo ya baadhi ya mitambo yake ya Ubungo I iliyopo mkoani Dar es Salaam inayozalisha Megawati 25.
 
Nyingine ni upanuzi wa mitambo ya Kinyerezi I  yenye uwezo wa kuzalisha Megawati 185, upanuzi wa mitambo ya Ubungo III Megawati 112, pamoja na kuwasha kituo cha Nyakato kinachozalisha Megawati 36 na hivyo kuongeza  jumla ya Megawati 358.
 
Taarifa  hiyo imeongeza kuwa,  mabadiliko  ya hali hewa na  kupungua kwa kiwango cha maji katika mito na mabwawa katika maeneo mbalimbali nchini kumeathiri uzalishaji wa umeme katika vituo vya kuzalishia umeme vinavyotumia maji.
 
TANESCO imevitaja vituo hivyo vya kuzalisha umeme vilivyoathirika kwa kiasi kikubwa kuwa ni Kihansi, Kidatu na Pangani, ambapo kuna upungufu wa uzalishaji wa takribani Megawati 345 za umeme, ambayo ni asilimia 21 ya uzalishaji wote.
 
Kwa mujibu wa TANESCO, kwa kuwa kutakuwa na upungufu wa umeme kwa baadhi ya mikoa  nchini,  taarifa zitatolewa kwa wakati ili wateja waweze kupanga kazi zao.