Familia: Maisha ya Mwl. Nyerere yalithamini kumcha Mungu

0
359

Chifu Japhet Wanzagi Nyerere ambaye ni kiongozi mkuu wa ukoo wa Burito, ukoo unaolea familia 13 ikiwemo ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere amesema wanakumbuka miaka 100 ya kuzaliwa kwa Mwalimu Nyerere kwa kuenzi utaratibu wa maisha yake ambayo yalithamini kumcha Mungu na kuishi katika haki kwa kumjali kila mtu.

Chifu Wanzagi ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika mdahalo wa kujadili Urathi wa Mwalimu Nyerere, ikiwa ni sehemu ya kuenzi maisha ya Mwalimu Nyerere kuelekea kumbukizi ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwake.

Ameeleza kuwa Hayati Mwalimu Nyerere alikuwa na utaratibu wa kuanza na sala nyumbani na mara nyingi alikuwa akianzia asubuhi kanisani, na alipomaliza ndipo alielekea ofisini wakati akiwa katika uongozi au shambani wakati alipokuwa ameng’atuka.

Kwa upande wake Neema Nyerere ambaye ni mmoja wa Wanafamilia ya Mwalimu ameeleza kuwa, waliweza kuishi kwa kuheshimu kila mtu pamoja na kupinga rushwa kutokana na misingi mizuri ya malezi ambapo walikuwa wakisisitizwa kumtii na kumcha Mungu.

“Tulikuwa tunalelewa kama Watanzania wengine bila upendeleo tukisisitizwa kujali, tunashukuru sana hilo kwamba katika malezi tuliyopewa, tulikuwa lazima kila jumapili tunatakiwa kwenda kanisani. Hii misingi ya kumcha Mungu imetusaidia sana katika maisha yetu,” amesema Neema Nyerere

Kuhusu nidhamu waliyorithi kutoka kwa Hayati Baba wa Taifa, Mwanafamilia huyo amesema walijifunza kuwa ukianza jambo lolote lazima ulikamilishe kwa kuwa wakati wa uhai wake Baba wa Taifa alikuwa na nidhamu ya kuanzisha jambo na kuhakikisha analikamilisha.