EU kuendelea kuwa mshirika wa maendeleo Tanzania

Ikulu Chamwino, Dodoma

0
138

Rais Samia Suluhu Hassan ameushukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala ya maendeleo ya jamii, na kuwekeza katika miradi ya miundombinu kupitia Benki ya Uwekezaji ya umoja huo.

Amesema katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita Tanzania na EU zimesaini makubaliano ya msaada wa Euro milioni 111.5, kwa ajili ya kuboresha miradi ya sekta ya nishati hasa matumizi ya majiko banifu, uongezaji thamani mazao ya nyuki, kuboresha mazingira ya biashara na kuimarisha usalama wa chakula.

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, wakati wa mazungumzo yake na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Charles Michel, mazungumzo yaliyofanyika kwa njia ya mtandao na kugusia masuala yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na EU.

Amesema Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya pia imetoa Euro milioni 50 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa baadhi ya viwanja vya ndege katika mikoa mbalimbali nchini.

Kuhusu mapambano dhidi ya corona, Rais Samia Samia Suluhu Hassan amemtaarifu Rais huyo wa Baraza la Umoja wa Ulaya kuwa tayari Tanzania imejiunga na Mpango wa Kimataifa wa ugawaji wa chanjo kwa nchi maskini (COVAX facility) na ina mpango wake wa Taifa wa kupambana na corona unaoainisha mahitaji ya nchi, hivyo itawasilisha mahitaji yake kwa EU ili kupata msaada.

Kwa upande wake Michel amemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Umoja wa Ulaya utaendelea kuwa mshirika muhimu na wa kimkakati wa maendeleo nchini Tanzania na kikanda.

Aidha amesema tayari EU inashirikiana na viwanda mbalimbali  vinavyozalisha chanjo dhidi ya corona  barani Afrika kwa kuvijengea uwezo,  na  iwapo Tanzania itahitaji msaada huo Umoja wa Ulaya uko tayari kuisaidia.