Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), – Biswalo Mganga amefuta kesi 59 zilizokua zikiendeshwa katika mahakama mbalimbali za mkoa wa Mbeya.
DPP Mganga amefuta kesi hizo mkoani Mbeya, wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Augustine Mahiga kwenye mikoa ya Kusini.
“Niliowafutia kesi nendeni mkawe Raia wema, msirudie makosa, badala yake mkawe Mabalozi wema mtakaofanya kazi kwa bidii ili kumuunga mkono Rais wetu mpendwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli katika kauli yake ya hapa kazi tu”, amesema DPP Mganga.
Wakati wa ziara hiyo, Balozi Mahiga pamoja na DPP Mganga wametembelea gereza la Ruanda mjini Mbeya pamoja na lile la Tukuyu wilayani Rungwe kwa lengo la kujionea hali halisi ya mazingira ya utoaji haki jinai katika magereza hayo na taasisi mbalimbali za haki jinai ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Polisi, Mahakama na Magereza.
Kwa upande wake Waziri Mahiga amewataka watu wote waliofutiwa mashtaka kutorudia makosa waliyoyatenda awali na badala yake watumie nguvu na akili walizonazo kuzalisha mali kwa maendeleo yao na familia zao pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.
Kwa mujibu wa kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini ana mamlaka ya kuwafutia mashtaka Watuhumiwa wa makosa ya jinai katika magereza mbalimbali nchini.
Hadi sasa DPP Mganga amefuta jumla ya kesi 120 akiwa katika ziara hiyo kwenye mikoa Mitatu, ziara inayofanywa na Waziri huyo wa Katiba na Sheria.