DOUBLE TROIKA ya SADC yakutana Dar es salaam

0
128

Mawaziri wa Mambo ya Nje pamoja na Mawaziri wa Ulinzi na vyombo vya ulinzi  kutoka Jumuiya ya Maendeleo  Kusini mwa Afrika (SADC), – DOUBLE TROIKA , wamekutana kwa dharura jijini Dar es salaam kujadili hali ya kisasa na amani katika  Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC).
 
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo wa dharura wa DOUBLE TROIKA inayojumuisha Troika ya Siasa na Troika ya Ulinzi na Usalama, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi  amesema kuwa, lengo la mkutano huo ni kuweka mikakati itakayosaidia kuimarisha amani DRC na kumaliza migogoro iliyodumu kwa miongo mingi.
 
Waziri Kabudi amesema kuwa, mkutano huo utazisaidia nchi za SADC zenye vikosi vya Ulinzi na Usalama huko DRC ambazo ni Tanzania, malawi na Afrika Kusini kuimarisha amani, na DRC kufanya tathmini na kukubaliana hatua za kuchukua ili vita na migogoro ya mara kwa mara inayoibuka katika Jamhuri hiyo ifikie tamati na amani ya kudumu ipatikane.
 
“Mkutano huu wa leo ni wa Troika ya Siasa na Troika ya Ulinzi na Usalama ambapo kupitia mkutano huu tunaamini kuwa tutafanya tathimini ya hali ya amani DRC na kukubaliana ni hatua gani za kuchukua,” amesema Profesa Kabudi.
 
Katika hatua nyingine Profesa Kabudi amesema kuwa, ndani ya kipindi cha mwaka huu amani na Demokrasia vimezidi kuimarika katika nchi za SADC, kutokana na baadhi ya nchi Wanachama kuendesha chaguzi zilizomalizika kwa amani akitolea mfano Msumbiji na Botswana.