Dola milioni 6 za SADC kujenga reli

0
106

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imetoa dola milioni sita za kimarekani kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi  wa reli ya kimataifa ya Mtwara mpaka Mbambabay.

Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Jamal Kassim Ali alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari, kando ya kikao cha SADC kinachohusisha Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

“jambo kubwa ambalo ningependa mjue ni kwamba katika mwendelezo wa vikao hivi wenzetu wa SADC wameweza kutupatia takribani dola milioni 6 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa reli ya Mtwara mpaka Mbambabay ambayo itajengwa ili kurahisisha na kuifungua Mtwara na kanda hii ya Kusini kiuchumi, na mpaka sasa tayari SADC wametupatia pesa hizo.” amesema Waziri Jamal.

Ameongeza kuwa  katika vikao vilivyopita mambo mbalimbali yamejadiliwa ikiwa ni pamoja na  kuanzishwa kwa mfuko wa maendeleo wa nchi Wanachama wa SADC, wenye lengo la kuchochea maendeleo katika nchi Wanachama  na kuzitaka nchi zote za Jumuiya hiyo kushirikiana kuhakikisha  mfuko huo unaendelezwa.

“Sisi kama Tanzania kama ambavyo tumekuwa vinara katika kuhakikisha masuala ya ukombozi wa SADC  kisiasa, sasa tunakwenda na ajenda hii tuwe vinara katika ukombozi wa kisiasa lakini pia ukombozi wa kiuchumi, tunaomba ushirikiano wa nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya SADC katika kufanikisha jambo hili.” amesema Waziri Jamal.