japan imetangaza kutenga Dola Bilioni Ishirini za Kimarekani kwa kipindi cha miaka mitatu kwa nchi za Bara la Afrika, ili kuziwezesha nchi hizo kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo itakayoleta mageuzi ya kiuchumi.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo mara baada ya kumalizika kwa siku ya kwanza ya mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Afrika (TICAD 7) unaoendelea katika mji wa Yokohama nchini Japan
na kuongeza kuwa mkakati wa Tanzania ni kuendeleza viwanda.
Amesema kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazozalisha malighafi zinazosafirishwa nje kwa ajili ya kuongezewa thamani, lakini kwa sasa imedhamiria kupitia viwanda kutumia malighafi zake kuzalisha bidhaa mbalimbali na hivyo kutengeneza ajira kwa watu wake.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa, tofauti na mikutano iliyotangulia, mkutano wa TICAD 7 kwa mara ya kwanza umeweka fursa ya kuwa na mpango kazi wa Yokohama, ambapo badala ya kuwa na maazimio pekee, sasa kutakuwa na fursa ya kuweka malengo vilevile kupima utekelezaji wake na upatikanaji wa fedha.
Akifungua mkutano huo wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika, Waziri Mkuu wa Japan, -Shinzo Abe amesema kuwa, Japan itaendelea kuchangia maendeleo ya Bara la Afrika kupitia programu mbalimbali za ushirikiano kwa kuimarisha rasilimali watu, elimu ya awali kwa watoto na kuboresha huduma za afya kwa wote.
Mkutano wa Saba wa TICAD ambao umebeba kaulimbiu ya Kuiendeleza Afrika kupitia Watu, Teknolojia na Uvumbuzi, unahudhuriwa na zaidi ya washiriki Elfu Nne pamoja na Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 44 za Afrika.