Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amesema wizara yake kwa kushirikiana na wizara ya Fedha na Mipango, ipo katika hatua za mwisho kumalizia mazungumzo na Benki ya Dunia ili kupata fedha za kutekeleza mradi wa uendelezaji wa jiji la Dar es Salaam (DMDP II).
Akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Kigamboni mkoani Dar es Salaam Dkt. Faustine Ndungulile aliyetaka kufahamu ni lini serikali itaanza utekelezaji wa mradi wa uendelezaji jiji la Dar es Salaam(DMDP II) na hasa kwenye maeneo ya wilaya ya Kigamboni, Waziri Bashungwa amesema mradi huo utaanza pindi taratibu za kupata fedha kutoka Benki ya Dunia zitakapokamilika.
Waziri Bashungwa amesema, kwa sasa taratibu za kupata fedha kwa ajili ya mradi wa DMDP II zinaendelea vizuri na fedha hizo zikipatikana zitatumika kuendelea miundombinu na miradi iliyokusudiwa katika mradi huo.
Kuhusu uendelezaji wa miundombinu ya barabara kwenye maeneo yaliyo chini ya halmashauri, Waziri Bashungwa ameziagiza halmashauri zote kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kujenga barabara hizo kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).