Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi, amewaapisha Viongozi aliowateua hivi karibuni kushika nyadhifa mbalimbali katika wizara za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dkt. Mwinyi amemuapisha Mussa Haji Ali kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu na Issa Mahafoudh Haji kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.
Wengine walioapishwa hii leo na Rais Dkt. Mwinyi ni Dkt. Habiba Hassan Omar kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi, Uwekezaji, Mikidadi Mbarouk Mzee kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ na Aboud Hassan Mwinyi kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango anayeshughulikia Fedha na Mipango.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla hiyo ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said.