Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi amemuapisha Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Hafla ya kumuapisha Maalim Seif imefanyika Ikulu jijini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi na wageni mbalimbali.
Akizungumza mara baada ya kumuapisha Maalim Seif, Dkt Mwinyi amewataka viongozi wengine na Wananchi wote wa Zanzibar kufikia maridhiano na kusahau yote yaliyopita kama walivyofanya wao viongozi wakuu.
Amesisitiza kuwa kinachotakiwa hivi sasa ni viongozi hao wa juu kushirikiana ili kuhakikisha wanawaletea wananchi maendeleo na kuondoa tofauti zao.
Kwa mujibu wa Dkt Mwinyi, atajadiliana na Makamu huyo kwa kwanza wa Rais kuhusu nafasi nyingine za uteuzi zilizobaki ikiwa ni pamoja na zile za Uwaziri na viti vya uwakilishi vya Rais.
Hafla hiyo ya kumuapisha Maalim Seif imehudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Jaji Mkuu wa Zanzibar, – Omar Othman Makungu na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Zubeir Ali Maulid.