Dkt. Mwinyi aitaka ZAECA kujitathmini

0
141

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kujitathmini utendaji kazi wake, kutokana na kuwepo kwa matukio kadhaa ya wizi wa mali za serikali na uhujumu uchumi.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu Zanzibar baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wa Zanzibar, inayoishia Juni 30 mwaka 2021.

Amesema ni muhimu kwa taasisi hiyo kujitathmini juu ya utendaji wake wa kazi, kwa kigezo kuwa kumekuwepo kesi nyingi za wizi wa mali za serikali na Uhujumu Uchumi, ambapo mbali na kukabidhiwa ili izishughulikie hakuna mrejesho kwa kipindi kirefu.

Rais Mwinyi amesema kinachosikitisha ni kuwa baadhi ya kesi hizo watuhumiwa wamekiri kuhusika na wengine kukubali kurejesha fedha serikalini, lakini hakuna hatua za kisheria zilizobainishwa kuchukuliwa.

Ametolea mfano tukio la wizi wa fedha lilitokea Bodi ya Mapato Zanzbar (ZRB) kupitia mtandao, ambalo hadi sasa halijaainishwa hatua zilizochukuliwa na kusema utamaduni huo umefanya vitendo kama hivyo kujirudia mara kwa mara.

Rais Mwinyi amempongeza CAG wa Zanzibar Dkt. Othman Abass Ali kwa moyo wa kujitolea na kubainisha kasoro mbalimbali zilioko katika wizara na taasisi za serikali.

“Laiti kama kazi inayofanywa na CAG ingefanywa na vyombo vyengine vinavyohusika, matukio kama haya yasingejirudia.” amesema Rais Mwinyi