Dkt. Mpango: Mapinduzi ya Zanzibar yachochee mapinduzi ya kijani

0
154

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema kwa sasa suala la upandaji miti linapaswa kuwa la lazima na kuziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafikia lengo la upandaji miti milioni moja na laki tano kwa mwaka kama ilivyopangwa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akiongoza zoezi la upandaji miti katika Jiji la Dodoma maeneo ya Ihumwa na Msalato ikiwa ni maadhimisho ya Miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na kuwa mapinduzi hayo yanapaswa kutumika kama chachu ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani na kurekebisha yale yote yaliofanyika katika kuharibu mazingira.

Aidha, amesisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi na wafanyabiashara katika upandaji na utunzaji miti pamoja na kuzisihi familia kuongeza juhudi katika upandaji miti na usafi wa mazingira.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka viongozi kuwa mfano katika zoezi la upandaji na utunzaji miti kwa kuonesha kwa vitendo na kila mwananchi anapaswa kuimwagilia miti iliyopandwa mbele yake hususani wale wanaomiliki vituo vya mafuta na wanaozalisha tofali.

Dkt. Mpango ametoa wito kwa Waandishi wa Habari hapa nchini kutoa kipaumbele katika kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya upandaji miti na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla kwani ni muhimu kutoa habari za mifano ya wale walioweza kutunza mazingira ili wawe hamasa kwa Watanzania wengine.