Dkt. Mpango kushiriki Jukwaa la Uwekezaji

0
211

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amewasili Abidjan, Ivory Coast, ambapo anamwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika litakalofanyika tarehe 2 hadi 4 mwezi Novemba mwaka huu.

Dkt. Mpango anatarajiwa kuongoza mazungumzo baina ya Tanzania na wawekezaji mbalimbali kuhusu uwekezaji katika miradi ya kimkakati nchini katika sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji, Usafirishaji na Uchukuzi.

Jukwaa la Uwekezaji Barani Afrika linaratibiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa kushirikiana na waanzilishi wa Jukwaa hilo na linalenga kuwakutanisha wawekezaji, sekta binafsi na sekta ya umma ili kuweka mikakati ya kufadhili miradi endelevu.

Jukwaa hilo linashirikisha wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, wakuu wa taasisi na mashirika ya kimataifa pamoja na wafanyabiashara.