Dkt. Mpango awakumbuka wenye mahitaji maalum

0
172

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amelishukuru Shirika la Teresia wa Mtoto Yesu lenye Makao Makuu yake nchini India kwa kazi nzuri linayofanya kuisaidia Tanzania katika kazi ya kuwatunza watoto yatima, wazee pamoja na watu wenye mahitaji maalum.

Dkt. Mpango ametoa shukrani hizo alipotembelea Kituo cha kuwatunza watoto yatima, wazee pamoja na watu wenye mahitaji maalum cha Huruma Missionary Sisters of Charity kiliopo Hombolo mkoani Dodoma.

Amesema kutokana na kazi nzuri inayofanywa kituoni hapo, atawaagiza maafisa wa wizara ya ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kitengo cha Ustawi wa Jamii kufika katika Kituo hicho, ili kuangalia namna ya kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali.

Akiwa kituoni hapo, Makamu wa Rais amewasilisha salam za Rais Samia Suluhu Hassan  ambaye amewatakia Watanzania wote heri ya sikukuu ya Pasaka na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Kwa sasa, Kituo hicho cha kuwatunza watoto yatima, wazee pamoja na watu wenye mahitaji maalum cha Huruma Missionary Sisters of Charity kinatunza takribani watu 90 wenye uhitaji wa aina mbalimbali.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amefika katika kituo hicho kinachosimamiwa na Shirika la Teresia wa Mtoto Yesu kwa lengo la kutoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwa ni.pamoja na chakula, sabun na fedha taslimu shilingi milioni 5.