Dkt Mpango awaagiza Viongozi wa Serikali kufanya kazi kama timu

0
296

Makamu wa Rais  Dkt Philip Mpango amewaagiza Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu kufanya kazi kama timu, na kila kiongozi kuthamini kazi ya msaidizi wake kwa maslahi ya Taifa.

Akizungumza Ikulu Chamwino mkoani Dodoma mara baada ya kuapishwa kwa Viongozi  mbalimbali walioteuliwa hapo jana na Rais Samia Suluhu Hassan, Dkt Mpango amesema tabia ya misuguano kati ya viongozi ndani ya wizara inarudisha nyuma maendeleo ya Taifa.

Kuhusu wajibu aliopewa na Rais Samia wa kusimamia masuala ya fedha kwa maslahi ya pande zote mbili za Muungano, Makamu wa Rais Mpango amesema hiyo ndio itakuwa kazi za mwanzo kwa wizara ya Fedha.

Dkt Mpango amemuagiza Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba kuhakikisha kuwa masuala hayo ya fedha ya pande mbili za Muungano yaliyokuwa ni moja kati ya kero za Muungano kuwa kazi ya kwanza atakayoifanya anapoanza kazi katika wizara hiyo.

Aidha amesisitiza kuongeza mbinu za kuongeza ukusanyaji wa mapato hadi kufikia shilingi Trilioni moja kwa mwezi.

Makamu wa Rais amesisitiza Wananchi wana matumaini makubwa kutokana na kasi ya Rais Samia katika kuwaletea maendeleo na kutimiza ndoto zilizoachwa na aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt John Magufuli