Dkt. Mpango atoa maelekezo kwa Waziri wa Mazingira

0
120

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amemuagiza waziri mwenye dhamana ya mazingira kwa kushirikiana na watumishi wote wa wizara hiyo kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi nchi nzima waweze kufahamu fursa zilizopo katika biashara ya hewa ukaa.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akikabidhi mfano wa hundi ya jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa halmashauri ya wilaya ya Tanganyika pamoja na vijiji nane vya wilaya hiyo fedha zilizotokana na biashara ya hewa ukaa.

Pia, ameitaka wizara kuhakikisha mapungufu ya kisera na usimamizi wa biashara ya hewa ukaa yanapatiwa ufumbuzi ili taifa liweze kunufaika na biashara hiyo.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa halmshauri zingine hapa nchini kujifunza kutoka Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi namna ya kufaidika na biashara hiyo, huku akiiagiza wizara ya maliasili na utalii kwa kushirikiana na serikali za mikoa kuwachukulia hatua kali za kisheria waharibifu wa mazingira ikiwemo wanaochoma moto misitu pamoja na kusimamia sera na sheria ya mazingira ili kupunguza na kuondoa athari za kimazingira zinazoweza kujitokeza.

Pia, ameagiza mkoa wa Katavi kufanya tathimini ya kimazingira na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa kushirikisha moja kwa moja jamii.