Dkt Mpango atembelea hifadhi ya Taifa ya Gombe

0
116

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango leo tarehe 28 Januari 2022 ametembelea hifadhi ya Taifa ya Gombe iliopo mkoani Kigoma.

Makamu wa Rais amejionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika hifadhi hiyo maarufu kwa upatikanaji wa Sokwe, pamoja na miti ya asili iliochanganyika kutoka Afrika ya kati na Afrika Afrika Mashariki.

Akiwa katika hifadhi hiyo Makamu wa Rais ametembelea maabara ya utafiti inayotumika kutafiti uzao wa sokwe na kutambua kizazi halisi cha sokwe hao.

Aidha Makamu wa Rais ametembelea nyumba alioishi mtafiti wa kwanza wa kimataifa wa Sokwe Dkt. Jane goodall alipokuwa hifadhini hapo.

Mkurugenzi wa utafiti wa taasisi ya Jane Goodall Dkt. Deus Kijungu pamoja na wahifadhi wa hifadhi hiyo wamemueleza Makamu wa Rais changamoto ya uharibifu wa mazingira inayofanywa na baadhi ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo pamoja na wale wanaotoka mataifa jirani. Aidha wamesema sokwe hao wamekuwa wakisumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya mlipuko yanayopelekea vifo vyao.

Akizungumza baada ya kutembelea hifadhi hiyo, Makamu wa Rais amewapongeza wahifadhi na watafiti waliopo katika hifadhi hiyo kwa jitihada kubwa wanazofanya kulinda sokwe waliopo hifadhini humo. Makamu wa Rais amewahimiza watafiti kujielekeza katika tafiti za kukabiliana na magonjwa yanayosumbua sokwe hifadhini hapo ili kupunguza hatari ya kupotea kwa sokwe hao wakati ujao.

Aidha Makamu wa Rais ameutaka uongozi wa mkoa wa Kigoma kutoa elimu pamoja na kupambana na vitendo vya uharibifu wa mazingira vinavyofanywa na wananchi waliopo maeneo jirani na hifadhi hiyo.

Amesema wakati wote ni muhimu kuzingatia taratibu za kuingia na kutoka katika hifadhi hiyo ili kupunguza hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoweza kuwapata sokwe hifadhini.

Makamu wa Rais amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuhamasisha utalii wa ndani utakaochochea ukuaji wa mapato pamoja na ulinzi wa hifadhi zilizopo nchini.

Amesema ni muhimu kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuwa mstari wa mbele na wa mfano katika kutembelea vivutio vya utalii ili kujua changamoto zilizopo na kuzitatua.