Dkt.Mpango ataka usimamizi sekta ya maji

0
244

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amezitaka mamlaka za maji pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo kuongeza weledi katika usimamizi wa rasilimali za maji.

Amesem ni muhimu zikajenga miundombinu mingi zaidi ya kutunza maji na kuvuna maji ya mvua ili kukabiliana na changamoto za maji ambazo hujitokeza.

Makamu wa Rais amesema hayo mkoani Shinyanga wakati akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji wa ziwa Victoria utakaohudumia Tinde na Shelui ambao utagharimu shilingi bilioni 24.4 hadi kukamilika kwake.

Amesema dhamira ya serikali ni kuona mradi huo unatoa maji na kuwa endelevu kwa wananchi kama ilivyokusudiwa na kwamba juhudi za kupeleka maji katika maeneo yaliyopo karibu na mradi huo zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuhakikisha maeneo yote yanapata majisafi na salama na yanatosheleza mahitaji.

Dkt. Mpango ameongeza kuwa sekta ya maji ni miongoni mwa sekta za kipaumbele katika mkakati wa kukuza uchumi wa viwanda na kupambana na umaskini nchini.

Kwa upande wake waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema wizara hiyo inatekeleza miradi ya maji ya kimkakati katika mkoa wa Shinyanga inayogharimu shilingi bilioni 35 ambayo itasaidia wananchi wa mkoa huo kuondokana na changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama.