Dkt. Mpango asisitiza tahadhari dhidi ya corona

0
182

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango anayeendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma, ametoa rai kwa Wakazi wa mkoa huo na Watanzania wote kuchukua tahadhari dhidi ya corona.

Ameutaja mkoa wa Kigoma kuwa ni moja ya mikoa yenye idadi kubwa ya maambukizi nchini, kutokana na uwepo wake katika mpaka na nchi jirani.

Kufuatia hali hiyo, Dkt. Mpango ameuagiza uongozi wa mkoa wa Kigoma kuhakikisha maeneo yote ya kutolea huduma za kijamii kunakuwepo na maji tiririka pamoja na watu wanavaa barakoa ili kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Uvinza utakaogharimu shilingi bilioni 3.8 hadi kukamilika kwake, Dkt. Mpango amewaagiza Watumishi wa hospitali hiyo kufanya kazi kwa uaminifu, na kuzingatia maadili ya kazi yao.

Amepongeza uanzishwaji wa duka la dawa katika hospitali hiyo na kutoa angalizo duka hilo lisiwe chanzo cha upotevu wa dawa hospitalini hapo, na ametaka wafuate maelekezo ya Serikali ya namna ya uendeshaji wa duka hilo.