Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango leo amemuwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu wa nne wa Dayosisi ya Western Tanganyika Askofu Emmanuel Charles Bwatta iliofanyika katika kanisa la Anglikana la mtakatifu Andrea lililopo Kasulu mkoani Kigoma.
Ibada hiyo imeongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Maimbo Mndolwa na kuhudhuriwa na maaskofu wa Dayosisi mbalimbali za Kanisa la Anglikana Tanzania na Burundi, Viongozi wa Dini zingine, Viongozi wa serikali, Chama na Wabunge wa mkoa wa Kigoma.
Akitoa salamu za serikali kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan , Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema Serikali ya Awamu ya Sita, inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Kanisa la Anglikana Tanzania, katika kuwahudumia watanzania kiroho na kimwili.
Makamu wa Rais amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi zote za dini nchini, ili kuziwezesha Taasisi hizo kuendelea kuwahudumia wananchi kiroho na kimwili kwa ufanisi zaidi.
Makamu wa Rais ametoa salamu za pongezi zake na kutoka wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Askofu Emmanuel Bwatta kwa kuwekwa wakfu na kutawazwa kuwa Askofu wa Nne wa Dayosisi ya Western Tanganyika.
Makamu wa Rais ameliomba Kanisa la Anglikana Tanzania pamoja na dini zingine kukemea na kutoa mafunzo ya kiroho kwa kufundisha kwa nguvu na mamlaka, maadili mema kwa vijana na watanzania kwa ujumla dhidi ya tamaa ya kujipatia mali haraka kwa njia zisizo halali.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amemsihi Askofu wa Dayosisi ya western Tanganyika kuimarisha ushirikiano baina ya Dayosisi hiyo na dini zingine,serikali na wananchi kwa ujumla ili kuharakisha maendeleo ya kanisa na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Askofu wa Dayosisi ya Western Tanganyika Emmanuel Bwatta ameishukuru serikali kwa kuendelea kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama hasa katika mkoa wa Kigoma kutokana na kumalizwa kwa vitendo vya uhalifu vilivyokuwa vikitokea wakati wa safari mbalimbali za kufika mkoani Kigoma.