Dkt. Mpango afungua kongamano la Kiswahili

0
154

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amefungua kongamano la pili la Idhaa za Kiswahili Duniani, ufunguzi uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Arusha (AICC).

Makamu wa Rais amewasihi wataalamu, mabingwa na wapenzi wa lugha ya Kiswahili kuendelea kuandika vitabu vya taaluma mbalimbali kwa lugha ya Kiswahili, ili kuepusha ongezeko la upotoshaji wa matumizi wa lugha ya Kiswahili miongoni mwa jamii husasani wanahabari wanaotumia maneno yasiyo rasmi au kuchanganya kiswahili na maneno ya lugha nyingine.

Amesema ubunifu unahitajika katika ufundishaji na uwasilishaji wa lugha ya Kiswahili kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ili kuendana na kasi ya maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Aidha amesema Katika tasnia ya habari, ni muhimu kuwa na vifaa bora vitakavyowezesha maarifa ya lugha ili yafike popote yanapohitajika kwa haraka na ufasaha.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo tayari kushirikiana na Taasisi na wadau mbalimbali katika kusimamia kwa karibu mkakati wa Taifa wa kubidhaisha Kiswahili ambao utazinduliwa rasmi siku ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani na kuhakikisha kuwa unatekelezwa kikamilifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Amesema Serikali itaendelea kuhamasisha ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni kupitia Balozi na kujenga ushawishi kwa nchi nyingine kuingiza lugha ya Kiswahili katika mitaala ili kuendelea kusambaza lugha hiyo.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema wizara itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wataalamu wa lugha ya kiswahili ili waweze kutumia fursa mbalimbali za lugha hiyo kama vile ukalimani, tafsiri, ufundishaji, uhariri na uandishi wa vitabu na majarida.

Ameongeza kwamba wizara imeandaa kanzi data ili kuwatambua wataalamu wa kiswahili nchini katika ngazi zote.

Kwa upande wake kaimu katibu mtendaji wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Consolata Mushi amesema Kongamano hilo litasaidia kubadilishana uzoefu na kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowapata wanahabari katika kutumia Kiswahili katika kazi zao.

Amesema uzinduzi wa Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la 3 utaongeza ufanisi katika tasnia ya habari kwa idhaa zinazotumia lugha ya Kiswahili, kutokana na uwepo wa maneno zaidi ya mia moja mapya.