Dkt. Magufuli aahidi kufanya kazi kama Mwalimu Nyerere

0
567


Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli amesema iwapo atapata ridhaa ya kuwa Rais kwa kipindi kingine cha miaka mitano ataendeleza yale yote ambayo Baba wa Taifa, Hayati Mwl. Julius Nyerere alitaka kuyafanya.

Dkt. Magufuli amesema hayo wakati akihutubia wananchi waliojitokeza katika eneo la Mukendo mkoani Mara ikiwa ni muda mfupi baada ya Mama Maria Nyerere kuzungumza na wananchi kwenye mkutano huo.

Mgombea huyo amesema kuwa licha ya kuwa Mwalimu Nyerere ameshafariki dunia lakini roho na mapenzi yake kwa Tanzania bado yapo.

“Ametuachia taifa lililo huru linalojiheshimu, lisilotishwa na mtu yeyote,” amesema Dkt Magufuli huku akiwasisitiza wananchi kusoma na kumuelewa kiongozi huyo aliyelikomboa taifa.

Kiongozi huyo tayari ametekeleza mambo kadhaa yaliyokuwa yakipigiwa chapuo na Mwalimu Nyerere ikiwa ni pamoja na kuhamishia serikali Dodoma ambapo ndipo Makao Makuu ya Tanzania na kuanza ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji katika Mto Rufiji.

Mbali na hilo, ameahidi kuendeleza Mkoa wa Mara na kujenga uwanja wa ndege ili ndege ambazo serikali inaendelea kununua ziruke moja kwa moja kutoka mkoani humo kwenda maeneo mbalimbali.

Dkt. Magufuli pia amewaasa wakazi wa Mara kuacha ukabila na kuwa na umoja kwa maendeleo yao.