Dkt Mabula ashangaa Mafia kuwa na Mtumishi Mmoja Idara ya Ardhi

0
144

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameagiza kupatiwa majina ya Watumishi Saba wa Idara ya ardhi, waliopangiwa kuhamia katika halmashauri ya wilaya ya Mafia mkoani Pwani lakini wameshindwa kuripoti kazini.

Dkt Mabula ametoa agizo hilo akiwa katika ziara yake ya siku Mbili wilayani Mafia, ziara yenye lengo la kuhamasisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya ardhi, kukagua mfumo wa ukusanyaji kodi ya ardhi kwa njia ya Kielektroniki, kukagua Masijala ya ardhi na kutatua migogoro ya ardhi.

Agizo la Naibu Waziri Mabula amelitoa baada ya Mkuu wa wilaya ya Mafia, – Shaib Nnunduma kumueleza kuwa, wilaya hiyo ina Mtumishi mmoja wa Idara ya ardhi jambo linalokwamisha utendaji kazi.

Amesema kuwa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi italishughulikia suala hilo haraka, kwa kuwa ni vigumu wilaya kufanya kazi vizuri katika Idara ya ardhi kwa kutegemea Mtumishi mmoja.

‘’Mafia mna Mtumishi mmoja wa sekta ya ardhi?, suala hili inabidi lifanyiwe kazi mapema, na wizara yangu italifanyia kazi kuhakikisha wilaya inakuwa na Watumishi wa njanja zote katika sekta ya ardhi’’, amesisitiza Dkt Mabula.